Skip to main content
Donate Now

Upembe na Afrika Mashariki: Uhalifu wa Kivita, Ukandamizaji wa Uchaguzi

Serikali Zinazohusika Zinapaswa Kuchukua Hatua Dhidi ya Makundi Yanayokiuka Haki na Kushinikiza Kulindwa kwa Uhuru wa Kiraia

Familia zilizofukuzwa kwao El-Fasher zikiwa kwenye kambi ya Tawila, eneo la Darfur, Sudan, Oktoba 31, 2025.  © 2025 Norwegian Refugee Council kupitia AP

(Nairobi) – Raia nchini SudanSudan Kusini, na Ethiopia wamekuwa ndio waathirika wakubwa kwenye migogoro ya kidhalimu inayokiuka haki ambapo pande zinazopigana zimekuwa, mara nyingi kwa makusudi, zinawalenga raia, Shirika la Human Rights Watch limesema leo katika Ripoti ya Dunia ya 2026. Serikali katika eneo zima zimekandamiza uhuru wa kiraia na kisiasa ambao tayari ulikuwa umezuiliwa watu hawawezi kujieleza kupitia maandamano hasa kabla uchaguzi.

“Mashambulio ya kikatili dhidi ya raia na vikosi vya kijeshi na makundi ya silaha bila kuwajibishwa ni jambo la kawaida katika Upembe wa Afrika na Afrika Mashariki, huku washikadau wa kimataifa na kanda wakiwa bado hawajawa tayari kuchukua hatua dhidi ya wahusika na wafuasi wao,” amesema Mausi Segun, Mkurugenzi Mtendaji wa Afrika wa Human Rights Watch. “Washikadau wa kikanda na wa kimataifa wanapaswa kuwaadhibu wahusika wanaokiuka haki, kuwawajibisha, na kudumisha ukaguzi huru wa haki za binadamu katika nchi hizi.”

Katika Ripoti ya Dunia 2026 yenye kurasa 529, toleo lake la 36, Human Rights Watch inachunguza mienendo ya haki za binadamu katika nchi zaidi ya 100. Katika taarifa ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji Philippe Bolopion anasema kuvunja wimbi la utawala wa kiimla linalosambaa duniani ni changamoto ya kizazi kimoja.

Anasema mfumo wa haki za binadamu uko chini ya tishio ambalo halijawahi kushuhudiwa kutokana na utawala wa Trump na mamlaka nyingine za kimataifa, na anazitaka demokrasia zinazoheshimu haki na asasi za kiraia kuunda muungano wa kimkakati wa kulinda uhuru wa msingi.

Kukithiri kwa ukiukaji wa sheria za kivita na kutokuwa na uwajibikaji kunafanyika nchini Sudan. Vikosi vya Rapid Support Forces, vinavyopigana na jeshi kwa ajili ya kudhibiti nchi, vilishambulia kambi kubwa zaidi ya wakimbizi katika eneo la Darfur, kuzingira mji mkuu wa North Darfur, El Fasher, na kufanya ghasia kubwa kwa kuteka mji huo mwezi Oktoba, na kufanya mauaji makubwa. Vikosi vya Jeshi la Sudan na washirika wake, hasa viliporejea kudhibiti majiji na miji mikuu muhimu, vililenga raia kwa makusudi na kuibomoa miundombinu ya kiraia kiholela.

  • Mgogoro umeibuka tena katika sehemu za Sudan Kusini ukiwa na athari kubwa kwa raia. Katika Upper Nile, mabomu ya anga yaliangushwa na serikali katika maeneo yenye watu wengi, ikiwa ni pamoja na mabomu ya kuwasha, ambayo yanaweza kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita, yalisababisha vifo na majeraha kwa mamia ya raia na kusababisha uhamisho mkubwa. Kufuatia kucheleweshwa kwa uchaguzi wa Sudan Kusini kwa mara nyingine, serikali ilidhoofisha zaidi haki na uhuru wa msingi kwa kuwazuilia na kuwahukumu viongozi wa vyama vya upinzani kwa makosa makubwa.
  • Vikosi vya serikali na wanamgambo wa Fano katika mkoa wa Amhara nchini Ethiopia vilitenda uhalifu wa kivita na ukiukaji mwingine mkubwa wa haki, huku vikosi vya Eritrea katika mkoa wa Tigray vikifanya ukiukaji dhidi ya raia katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao. Kwa kuwa uchaguzi umepangwa Juni 2026, mamlaka yalilenga waandishi wa habari na vyombo huru vya habari na kujaribu kuhalalisha ukandamizaji wao kwa mashirika ya haki za binadamu.

Serikali katika eneo hilo zimekandamizaji pakubwa uhuru wa kiraia, hasa uhuru wa watu kuandamana na kuhusika kwa uchaguzi bila kuzuiwa.

  • Vikosi vya usalama vya Kenya vilivuruga maandamano kwa ukatili kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kutenda ukiukaji mwingine mkubwa dhidi ya waandamanaji.
  • Nchini Tanzania na Uganda, kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa Oktoba 2025 na Januari 2026 mtawalia, mamlaka yaliwazuilia viongozi muhimu wa upinzani, yakakandamiza waandishi wa habari na waandamanaji, na kudhoofisha haki za uhuru wa kujieleza.
  • Mamlaka ya Tanzania yalikabili maandamano ya siku za uchaguzi kwa ukatili vikitumia nguvu kupita kiasi na ukiukaji mwingine, kukiwamo kuzima mtandao wa mawasiliano kote nchini.
  • Licha ya uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba ni kinyume cha katiba, Uganda iliruhusu tena kufanyika kwa kesi za raia katika mahakama za kijeshi, zikilenga wapinzani wa kisiasa.
  • Licha ya mamlaka yao ya kuzuia na kupunguza migogoro, Umoja wa Afrika na vyombo vya kikanda, likiwamo Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), havikuchukua hatua yoyote yenye maana ya kulinda raia, kuzuia ukiukaji, au kuwawajibisha wahalifu.

Human Rights Watch ilisema serikali zinapaswa kuchukua hatua dhidi ya makamanda wa vikosi vinavyotumia ukatili, kuunga mkono vyombo huru vya habari na jamii, na kusaidia mashirika ya kikanda na ya kimataifa kuhakikisha uchunguzi na uwajibikaji unafanywa.

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.